Image caption Viongozi wa Chadem Mahakamani

Mahakama kuu jijini Dar es Salam Tanzania imewakuta na hatia viongozi tisa wa upinzani kwa makosa 12 kati ya 13 ambayo walishtakiwa Februari, 2018.

Makosa hayo ni pamoja na kuitisha maandamano bila kibali na kusababisha vurugu.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe pamoja na viongozi wenzake wametakiwa kulipa faini ya shilingi milioni 350 za Tanzania ambazo ni sawa na dola elfu kumi na tatu.

Wakosoaji wameishutumu serikali kwa kutumia mahakama kama njia ya kuua upinzani nchini humo kwa kuwapa kesi viongozi wake.

  • Je, Mbowe kuuvusha upinzani Tanzania?
  • Viongozi wa Chadema wana kesi ya kujibu

Mapema Jumanne kulishuhudiwa tukio la patashika katika maeneo ya karibu ya mahakama kabla ya hukumu hiyo kusikilizwa.

Wanachama wa upinzani walifurika katika viwanja vya mahakama huku wengine wakiwa wanapiga magoti na kuimba wimbo wa ukombombozi kwa viongozi wao.

Polisi iliwabidi watumie nguvu kuwatawanya wanachama hao na kuwakamata baadhi yao ili kufanya eneo hilo la mahakama liwe wazi.

Kwa hali ambayo haijazoeleka, Muendesha mashtaka wa kesi hiyo aliingia mahakamani akiwa analindwa na polisi watatu.

Baada ya kusoma mashtaka yao, Jaji Thomas Simba aliwakuta hatiani kwa makosa kumi na mbili kati ya 13 ambayo walikuwa wanashitakiwa ambayo kikubwa walisabisha vurugu na kufanya mikutano ya hadhara bila ruhusa.

Washitakiwa wote tisa ambao ni viongozi wa Chadema wametakiwa kulipa faini au kwenda jela kwa kipindi cha miezi mitano kila mmoja.

Image caption Chama cha upinzani Tanzania-CHADEMA kimeomba wanachama wake kuwasaidia katika kulipa faini waliyopewa

Wanasiasa wa upinzani na wanachama wao wanasema kuwa hukumu hiyo imetolewa kwa mlengo wa kisiasa.

Mamlaka ya Tanzania imekuwa ikilaumiwa kuwadhalilisha wapinzani katika mahakama.

Na uhuru wa kisiasa umeshuka mara baada ya John Magufuli kuingia madarakani mwaka 2015, lakini serikali ilikanusha madai hayo.